Habari
NIRC MBIONI UJENZI BWAWA LA KUVUNA MAJI YA UMWAGILIAJI BONDE LA EYASI
📍NIRC Karatu, Arusha.
Serikali kupitia Tume ya Taifa ya Umwagiliaji imewahakikishia wakulima skimu ya Umwagiliaji Mang'ola Barazani iliyopo wilayani Karatu Mkoani Arusha ipo mbioni kumpata mkandarasi kwa ajili ya ujenzi wa bwawa la Umwagiliaji litakalotumika kuvuna maji na kudhibiti mafuriko bonde la Eyas Wilayani Karatu mkoani Arusha.
Hayo yamejiri wakati wa mkutano wa wakulima wa skimu hiyo na wataalamu wa Tume, ambapo Mhandisi wa Umwagiliaji Mkoa wa Arusha William Simon amesema ujenzi wa bwawa hilo utasaidia kudhibiti mafuriko na kuvuna maji kwa kilimo cha Umwagiliaji.

Amesema azma ya Serikali ni kuhakikisha wakulima wanakuwa na Kilimo chenye tija na kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.
Amesema sambamba na ujenzi wa bwawa hilo Serikali pia imewekeza kiasi cha Shilingi bilioni 38 kwa ajili kuendeleza Skimu hiyo kwa kujenga miundombinu ya Umwagiliaji.
Paul Gutti, ni miongoni mwa wakulima wa skimu hiyo amebainisha kuwa wamekuwa wakikabiliwa na changamoto ya mafuriko kwa muda mrefu yaliyokuwa yakichangia uharibifu wa miundombinu ya Umwagiliaji pamoja na mazao hali inayosababisha kuzorota kwa shughuli za Kilimo kwa wakulima wa eneo hilo.

Amesema pamoja na ujenzi huo wa bwawa ujenzi wa miundombinu ya Umwagiliaji unaendelea n matarajio ni utekelezaji wake uweze kuleta tija kwa kuwa maji yatafika mashambani na kuepusha migogoro baina ya wakulima katika mgawanyo wa maji.
Hata hivyo mkutano huo wa wakulima umehusisha utiaji saini mkataba wa Uendeshaji, Usimamizi na Matunzo ya skimu unaolenga kuhakikisha miundombinu inayoendelea kujengwa inalindwa dhidi ya uharibifu.
Zoezi la utiaji saini mkataba huo ni utekelezaji wa mradi wa Mifumo Himilivu ya Chakula nchini (TFSRP-P4R).

Skimu ya Umwagiliaji Mang'ola Barazani ina ukubwa wa ekari 2850, ambapo eneo linalomwagiliawa kwa sasa ni ekari 700, huku kukamilika kwa mradi huo kutaongeza eneo la Umwagiliaji kufikia ekari 2211, huku kijiji kitakachonufaika ni Mang'ola Barazani, ambapo mazao yatakayolimwa ni vitunguu, mahindi, mpunga na maharage.


