Huduma Yetu
UENDESHAJI, USIMAMIZI NA MATUNZO YA MIUNDOMBINU YA UMWAGILIAJI

Tume ya Taifa ya Umwagiliaji (NIRC), kupitia Idara ya Uendeshaji, ina jukumu la kuhakikisha kuwa skimu zote za umwagiliaji nchini zinaendeshwa kwa kuzingatia Sheria ya Taifa ya Umwagiliaji, kanuni zake, na malengo ya kimkakati ya Tume. Jukumu hili linahusisha utoaji wa Miongozo ya kitaalamu na usimamizi wa utekelezaji wa shughuli za umwagiliaji kwa Vyama vya Wakulima Wamwagiliaji (Irrigators’ Organizations – IOs), Ofisi za Umwagiliaji za Wilaya (District Irrigation Offices – DIOs), na Ofisi za Umwagiliaji za Mikoa (Regional Irrigation Offices – RIOs).
Uratibu wa Mikataba ya OMM.
Idara inaratibu maandalizi na usainishaji wa Mikataba ya Uendeshaji, Usimamizi na Maintenance (Operation, Management and Maintenance – OMM) kati ya NIRC na IOs. Mikataba hii huainisha majukumu, haki, viwango vya huduma, na viashiria vya utendaji. Marekebisho hufanyika mara kwa mara kwa kuzingatia matokeo ya ufuatiliaji na tathmini ili kuhakikisha ufanisi endelevu.
Kujenga Uwezo wa Wadau.
Kwa kushirikiana na DIOs na RIOs, Idara huandaa na kusimamia mafunzo kwa Kamati za Usimamizi na Kamati Ndogo za IOs. Aidha, hutoa nyenzo muhimu kama vile miongozo ya OMM, mwongozo wa mgao wa maji, na nyaraka za marejeo ya kiufundi ili kuhakikisha uendeshaji sahihi wa skimu.
Ufuatiliaji na Tathmini ya Utendaji.
Idara hufuatilia utekelezaji wa mikataba ya OMM na kutathmini utendaji wa skimu kwa kutumia viashiria muhimu. Taarifa na takwimu hukusanywa kupitia Fomu Na. 1 hadi Na. 12 ambazo huonyesha rekodi za uendeshaji, shughuli za matunzo na taarifa za kifedha. Matokeo hutumika kutoa mapendekezo ya maboresho katika usimamizi wa skimu.
Usimamizi wa Mapato na Uwajibikaji wa Kifedha.
Idara inahakikisha utoaji wa ankara za Ada ya Huduma ya Umwagiliaji (Irrigation Service Fee – ISF) kwa Vyama vya Wamwagiliaji (IOs) au wanachama wao, ukusanyaji wa mapato kwa uwazi, na uzingatiaji wa kanuni za kifedha. Fedha zinazokusanywa huingizwa kwenye akaunti za NIRC kupitia namba za malipo zilizotolewa na Serikali.
Utunzaji na Usimamizi wa Mali za Wamwagiliaji.
Idara husaidia Vyama vya Wamwagiliaji (IOs) katika kuhifadhi kumbukumbu na kutunza mali muhimu kama milango, mifereji, na pampu. Pia hutoa mwongozo wa taratibu za ukaguzi na kushiriki katika ukaguzi wa ndani na wa nje ili kuhakikisha uwajibikaji wa kifedha.
Usimamizi wa Mazingira na Jamii.
Idara huhakikisha kuwa miradi ya maendeleo ya umwagiliaji inazingatia miongozo ya usimamizi wa mazingira, ikiwemo udhibiti wa uchafuzi, uhifadhi wa mifumo ya ikolojia, na matumizi endelevu ya maji. Pia huhamasisha mgao wa maji kwa usawa na kuwezesha mifumo ya utatuzi wa migogoro katika jamii za umwagiliaji.
Ushirikiano na Wadau.
Idara hushirikiana kwa karibu na Vyama vya Wamwagiliaji (IOs), Mamlaka za Serikali za Mitaa (Local Government Authorities – LGAs), na wadau wa maendeleo katika kuendeleza, kukarabati na kuboresha skimu za umwagiliaji. Aidha, inasisitiza mipango shirikishi, ufuatiliaji na tathmini jumuishi ili kuhakikisha maendeleo endelevu na ya usawa katika sekta ya Umwagiliaji nchini.
Kutoa elimu ya mbinu bora za kilimo kwa mazao yanayolimwa katika skimu za Umwagiliaji.
Idara kupitia maafisa kilimo waliopo katika ofisi za Umwagiliaji za Wilaya na mikoa inawajengea uwezo wakulima katika skimu za umwagiliaji kuhusu mbinu bora za kilimo cha mazao yanayozalishwa katika skimu za Umwagiliaji ili wakulima waweze kuzalisha kwa tija, kuboresha kipato na hatimaye kuchangia katika usalama wa chakula nchini.