Habari
MBUNGE MALINYI AIPONGEZA NIRC, WAKULIMA WA ITETE WASAINI MKATABA WA USIMAMIZI WA SKIMU
š Skimu ya Itete, Malinyi.
Wakulima wa Skimu ya Umwagiliaji Itete iliyopo Kijiji cha Alabama, Kata ya Itete, Wilaya ya Malinyi, Mkoa wa Morogoro, wameendelea kunufaika na juhudi za Serikali baada ya kushiriki mafunzo ya kuwajengea uwezo katika kilimo chenye tija na manufaa pamoja na kusaini mkataba wa Usimamizi, Uendeshaji na Matunzo ya skimu kupitia Mradi wa Mifumo Himilivu ya Chakula nchini (TFSRP-P4R).
Akizungumza katika mkutano wa wakulima wa skimu ya Umwagiliaji Itete Mbunge wa Jimbo la Malinyi Dkt. Mecktrids Mdaku ameishukuru Serikali kupitia NIRC kwa kuwakumbuka wananchi wa Malinyi, akieleza kuwa licha ya kuwepo kwa zaidi ya miradi 3,000 ya umwagiliaji inayotekelezwa nchini, Malinyi ni miongoni mwa maeneo yanayonufaika na uwekezaji huo mkubwa wa Serikali.
_1768298721.jpeg)
Dkt.Mecktrids amesifu hatua ya wakulima wa Itete kwa kuupokea vyema mradi huo wa Serikali pamoja na kuonesha utayari wa kujifunza na kupewa elimu sahihi ya Usimamizi, Uendeshaji na Matunzo ya skimu, akisisitiza kuwa utunzaji wa miundombinu ni msingi wa mafanikio ya mradi wowote wa maendeleo.
“Mradi wowote ukiutunza unakupa matokeo chanya, lakini mkiuacha uendee ndivyo sivyo, kwasababu serikali ipo itakuja kukarabati Ina kuwa siyo,” amesema Mbunge huyo.
Akizungumza katika mkutano huo, Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Uendeshaji kutoka Tume ya Taifa ya Umwagiliaji, Bi. Salome Njau, alisema lengo la NIRC kufika Itete ni kuwajengea wakulima uwezo na kuwaeleza kwa kina wajibu wa kila mwanachama wa skimu kuanzia uongozi hadi mkulima mmoja mmoja, ili kulinda na kutunza miundombinu ya umwagiliaji kwa manufaa ya sasa na ya vizazi vijavyo.
_1768298795.jpeg)
Amesema Serikali imewekeza fedha nyingi katika miradi ya umwagiliaji, na bila kuwepo kwa matunzo endelevu, miundombinu hiyo haiwezi kudumu wala kuleta matokeo yaliyokusudiwa.
“Nasisi tumekuja kuwa eleze ni kazi zipi za matunzo wanapaswa kuzifanya ili mradi huo uwafaidishe kuongeza uzalishaji lakini pia kuongeza kipato na pia tuone maisha ya wanaitete yanabadilika ndio Lengo kuu la serikali,” amesema Njau.
Aidha, ameongeza kuwa kufanikisha malengo hayo, NIRC imeingia makubaliano ya kisheria na wakulima kupitia mkataba wa Usimamizi, Uendeshaji na Matunzo ya skimu, unaoeleza kwa uwazi namna miundombinu ya umwagiliaji itakavyoendeshwa, kusimamiwa na kutunzwa.
Kwa upande wao, wakulima wa Skimu ya Umwagiliaji Itete wameishukuru Serikali kwa jitihada zinazoendelea kufanywa, huku wakisisitiza umuhimu wa uwajibikaji na ushirikiano wa pamoja kati ya viongozi na wakulima katika kutekeleza majukumu ya skimu.
“Leo tunaweza kukubaliana kiutendaji na tukasaini mkataba wa utekelezaji wake, serikali inatupenda inatoka fedha nyingi lakini utekelezaji unakuwa mgumu,” amesema Mkulima.
Pamoja na pongezi hizo, wakulima wameeleza changamoto ya ukosefu wa miundombinu bora ya barabara ndani ya skimu, hali inayosababisha gharama kubwa wakati wa uondoaji wa mazao kipindi cha mavuno.
Aidha kwa upandewake, Mhandisi wa Wilaya ya Malinyi, Bw. Noel Emmanuel alikiri kuwa hali ya barabara ndani ya skimu siyo nzuri, lakini aliwahakikishia wakulima kuwa kupitia mradi wa ukarabati wa Skimu ya Itete unaoendelea, barabara zote zitafanyiwa marekebisho ili kurahisisha usafirishaji wa mazao kutoka mashambani hadi sokoni.
“Huu mradi umekuja kama neema niwaahidi hizi changamoto tunazochukua na huu mradi unaokuja unakuja kumuongezea NGUVU mkandarasi,” amesema Noel.
Ujenzi na ukarabati wa Skimu ya Umwagiliaji Itete unaendelea, huku Serikali ikitarajia mradi huo kuongeza tija katika uzalishaji wa mazao na kuboresha maisha ya wakulima wa eneo la Itete kwa ujumla.
_1768299387.jpeg)

