Habari
BILLION 19.4 KUIMARISHA MIUNDOMBINU YA UMWAGILIAJI SKIMU YA LUNDO
📍Nyasa, Ruvuma
Serikali kupitia Tume ya Taifa ya Umwagiliaji inaendelea kuimarisha miundombinu ya Umwagiliaji katika skimu ya Lundo iliyopo Kijiji cha Lundo, Kata ya Lipingo wilayani Nyasa mkoani Ruvuma kupitia mradi wenye thamani ya takribani shilingi bilioni 19.4 unaolenga kuboresha upatikanaji wa maji ya uhakika kwa wakulima na kuongeza uzalishaji wa mazao.
Hadi sasa skimu hiyo inawanufaisha wakulima wapatao 524 wakiwemo wanaume 220 na wanawake 304 , huku eneo la takribani hekta 100 zinamwagiliwa na kukamilika kwa mradi huo utaongeza eneo la kumwagiliwa ili lengo la kuongeza uzalishaji wa mazao na kuboresha shughuli za kilimo kwa wakulima wa eneo hilo linafikiwa.
Katika hatua ya kuimarisha usimamizi wa miundombinu hiyo, wakulima wa skimu ya Lundo wamesaini mkataba wa uendeshaji, usimamizi na matunzo ya miundombinu ya Umwagiliaji kati yao na Tume ya Taifa ya Umwagiliaji ili kuhakikisha miundombinu hiyo inatunzwa na kutumika kwa ufanisi kwa manufaa ya wakulima wa sasa na vizazi vijavyo.
Akizungumza katika mkutano huo, Afisa Maendeleo ya Jamii kutoka Tume ya Taifa ya Umwagiliaji Heaven Jesse, amesema ushirikishwaji wa wakulima ni jambo muhimu katika utekelezaji wa miradi ya Umwagiliaji ili kuhakikisha miundombinu inayojengwa inaleta matokeo chanya kwa wakulima.
_1773807852.jpeg)
Amesema, katika utekelezaji wa mradi huo wakulima watahusishwa kikamilifu kupitia uundwaji wa kamati ya ujenzi ambayo itakuwa kiunganishi kati ya wakulima, mkandarasi pamoja na wataalamu wa Serikali katika kusimamia maendeleo ya mradi huo.
“Tunatambua kuwa mkulima ndiye mtaalamu wa kwanza wa eneo lake kwa sababu anafanya kazi shambani kila siku, hivyo ushiriki wenu ni muhimu ili kuhakikisha miundombinu inayojengwa inakidhi mahitaji halisi ya wakulima,” amesema Jesse.
Kwa upande wake Mhandisi wa Umwagiliaji Wilaya ya Nyasa kutoka Tume ya Taifa ya Umwagiliaji Elibariki Mwendo, amesema mradi huo unahusisha ujenzi wa miundombinu ya kisasa ya Umwagiliaji ikiwemo banio la kisasa la kuchukua maji, mifumo ya mifereji ya kupeleka maji mashambani na mifereji ya kutoa maji ya ziada ili kulinda mashamba dhidi ya mafuriko.

Ameeleza kuwa, hatua nyingine inayotekelezwa ni kunyoosha mkondo wa mto unaosababisha mafuriko ili kuhakikisha maji yanapita katika njia sahihi na kulinda mashamba pamoja na miundombinu ya Umwagiliaji inayojengwa.
“Lengo la miundombinu hii ni kuhakikisha wakulima wanapata maji ya uhakika kwa ajili ya kilimo cha Umwagiliaji pamoja na kulinda mashamba dhidi ya mafuriko yanayojitokeza wakati wa msimu wa mvua,” amesema Mwendo.
Baadhi ya wakulima wa skimu hiyo wameeleza matumaini yao kuhusu utekelezaji wa mradi huo wakiamini kuwa utasaidia kuboresha shughuli za kilimo katika eneo hilo.

Mkulima wa skimu ya Lundo Clement Njinga amesema wakulima wanatarajia mradi huo kusaidia kupunguza changamoto ya mafuriko ambayo mara nyingi huathiri shughuli za kilimo katika mashamba yao hasa wakati wa msimu wa mvua.
Kwa upande wake mkulima Fatma Ngonyani ameishukuru Serikali kupitia Tume ya Taifa ya Umwagiliaji kwa kuleta mradi huo, akisema utarahisisha shughuli za kilimo kwa wakulima hususan wanawake ambao hapo awali walilazimika kutumia nguvu kubwa kutengeneza mifereji ya maji kwa mikono.
Amesema ujenzi wa miundombinu ya kisasa ya Umwagiliaji utasaidia kuongeza uzalishaji wa mazao pamoja na kurahisisha shughuli za kilimo katika skimu hiyo.

