Habari
DKT. MASIKA ARIDHISHWA UTEKELEZAJI MRADI WA MEMBE

Mwenyekiti Bodi ya Uongozi Tume ya Taifa ya Umwagiliaji Dkt. Richard Masika amekiri kuridhishwa na hatua zinazofanywa na Tume katika utekelezaji miradi ya umwagiliaji ikiwemo mradi wa ujenzi bwawa la umwagiliaji Membe lililopo wilayani Chamwino mkoani Dodoma.
Dkt. Masika ametoa kauli hiyo mara baada ya kufanya ziara katika bwawa hilo ambapo kwa sasa ujenzi wake umefikia asilimia 86 ya utekelezaji wake.
Aidha Dkt. Masika ametoa wito kwa wakulima ambao ni wanufaika wa mradi huo kutoa ushirikiano kwa wataalamu wanaotekeleza mradi huo wakati wa ujenzi na mara baada ya mradi huo kukamilika, kuhakikisha mradi huo unafanikiwa na kuleta tija kwa wakulima.
Sanjari na hayo, Dkt. Masika ameielekeza Tume kuhakikisha kuwa katika utekelezaji wa mradi huo Tume inazingatia muda wa utekelezaji wa mradi na thamani ya ya mradi iendane na utekelezaji.
Akimwakilisha Mkurugenzi Mkuu Tume ya Taifa ya Umwagiliaji, Mkurugenzi Idara ya Mipango, Ufuatiliaji na Tathmini, Dkt. Consolatha Kapinga amekiri kupokea maelekezo ya Mwenyekiti huyo wa bodi na kuahidi kuyafanyia kazi na kuhakikisha mradi unakamilika kwa wakati ili kuleta manufaa kwa wananchi wa Dodoma na Taifa kwa ujumla.
Akizungumza kwa niaba ya wakulima wanufaika wa mradi huo, kaimu mwenyekiti kijiji cha Membe, Samweli Malima, ameishukuru serikali kwa kuendelea kuhakikisha mradi huu unakamilika, kwani utachangia kukuza kipato cha wakulima wa Membe hasa kundi la vijana ambao watajishughilisha na kilimo.
Mradi wa ujenzi wa Bwawa la Membe, unaotekelezwa na mkandarasi NAKUROI INVESTMENT CO. LTD, umefikia asilimia 86 ya utekelezaji. Bwawa hilo lenye thamani ya Shilingi bilioni 16.26, litawanufaisha wakulima 1,500 katika eneo la hekta 2,500. Miongoni mwa kazi zilizokamilika ni ujenzi wa tuta la bwawa (84%), ukuta wa zege (87%), na mfumo wa kutolea maji (92%).
Katika hatua nyingine, mradi wa skimu ya umwagiliaji Membe unaotekelezwa na mkandarasi CRJE EAST AFRICA LTD umefikia asilimia 25.5 ya utekelezaji wake.
Mradi huu wenye thamani ya Shilingi bilioni 19.39 unatarajiwa kunufaisha wakulima 2,150 katika eneo la hekta 2,900. Hata hivyo, baadhi ya kazi kama ujenzi wa mifereji ya kutolea maji bado hazijaanza.
Sambamba na miradi ya umwagiliaji, serikali inatekeleza mradi wa ujenzi wa nyumba 75 katika Skimu ya Membe, mradi huu wa Shilingi bilioni 6.69 unaendelea kwa kasi, ambapo misingi ya nyumba 62 imekamilika, huku nyumba 13 zikiendelea na maandalizi ya umwagaji wa zege.