Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Tume ya Taifa ya Umwagiliaji

Habari

SKIMU YA UMWAGILIAJI DUMBECHANDĀ  KULETA KILIMO CHENYE TIJA KWA WAKULIMA


šŸ“ Karatu, Arusha.

Serikali kupitia Tume ya Taifa ya Umwagiliaji inaendelea zoezi la uendelezaji eneo la Umwagiliaji katika Bonde la Eyasi lililopo wilayani Karatu Mkoani Arusha kwa kutekeleza mradi wa ujenzi wa Skimu ya Umwagiliaji ya Dumbechand, ikiwa miongoni mwa skimu saba zinazoendelezwa katika Bonde hilo.

Akizungumza katika mkutano wa wakulima wa skimu hiyo, Mhandisi Umwagiliaji Wilaya ya Karatu, Speciosa Roman, amesema wilaya hiyo imebahatika kunufaika na mradi mkubwa wa ujenzi wa skimu za Umwagiliaji unaotekelezwa katika hilo, ambapo zaidi ya Shilingi bilioni 38 zitatumika kuendeleza bonde hilo, huku Skimu ya Dumbechand ikitekelezwa kwa gharama ya Shilingi bilioni 4.

Amesema mradi huo unahusisha ujenzi wa miundombinu Umwagiliaji, barabara za mashambani, vigawa maji, makaravati pamoja na vitega maji, hatua itakayosaidia kuondoa changamoto ya  upungufu wa maji, kudhibiti mchanga kujaa kwenye mifereji na kukabiliana na migogoro katika mgawanyo wa maji, hivyo kuongeza tija ya uzalishaji.

Kwa upande wake, Mhandisi Mkazi wa Tume ya taifa ya Umwagiliaji Skimu ya Dumbechand, Meshack Lema, amesema mradi huo umezingatia mahitaji ya wakulima na wafugaji kwa kujenga makaravati katika maeneo yote yanayokatiza mifereji, barabara za mashambani pamoja na josho la kunyweshea mifugo, ili kuzuia mifugo kuingia kwenye miundombinu ya Umwaguliaji.

Nao wakulima wa skimu hiyo, kupitia Pius Petro, wamesema mradi huo utakuwa na manufaa makubwa kwao kwa kupunguza upotevu wa maji, kuongeza tija ya kilimo na kuinua kipato cha wakulima, huku wakiiomba Serikali kuendelea kuwapatia miradi mingine ikiwemo ujenzi wa visima kwa ajili ya Umwagiliaji.

Aidha kwa upande wake Afisa Kilimo Tume ya Taifa ya Umwagiliaji Emmanuel Lukombeso amewasihi wakulima kuendelea kutunza miundombinu ya Umwagiliaji, akibainisha kuwa kuingiza mifugo kwenye skimu ni miongoni mwa sababu kuu zinazosababisha uharibifu wa miundombinu hiyo.

Skimu ya Dumbechand hutegemea chanzo cha maji ambacho ni chemchem ya Qang’dand, huku mazao yanayolimwa katika skimu hiyo ni mahindi na vitunguu.