Habari
WAKULIMA WA ILEMBA WAASWA KUSIMAMIA VIZURI SKIMU BAADA YA KUSAINI MKATABA
📍Skimu ya Ilemba, Rukwa
Serikali kupitia Tume ya Taifa ya Umwagiliaji imeendelea kuimarisha usimamizi wa skimu za Umwagiliaji nchini kwa kushirikisha wakulima moja kwa moja katika uendeshaji, usimamizi na matunzo ya miundombinu.
Hatua hiyo imejidhihirisha katika skimu ya Umwagiliaji ya Ilemba wilayani Sumbawanga mkoani Rukwa ambapo wakulima wamesaini mkataba wa kusimamia na kutunza miundombinu ya Umwagiliaji inayojengwa katika eneo hilo.
Akizungumza na wakulima wakati wa kusaini mkataba huo, Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Uendeshaji kutoka Tume ya Taifa ya Umwagiliaji, Salome Njau, amesema Serikali imewekeza zaidi ya shilingi bilioni 21 katika mradi wa Umwagiliaji wa Ilemba ili kuboresha kilimo na kuongeza uzalishaji wa mazao.

Amesema uwekezaji huo, unalenga kuhamasisha wakulima kuachana na kilimo cha kutegemea mvua na kuingia kwenye kilimo cha Umwagiliaji ambacho kinaweza kufanyika muda wote wa mwaka na kuongeza tija kwa wakulima.
Ameongeza kuwa, kupitia mkataba huo wakulima watahusika kikamilifu katika kusimamia matumizi sahihi ya maji, kutunza miundombinu ya Umwagiliaji pamoja na kushiriki katika shughuli za uendeshaji wa skimu kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.
Kwa upande wake Afisa Kilimo kutoka Tume ya Taifa ya Umwagiliaji Emmanuel Lukombeso, amesema Serikali imeweka mkakati wa kuhakikisha sekta ya kilimo inachangia asilimia kumi ya pato la taifa ifikapo mwaka 2030 kupitia uwekezaji mkubwa katika miradi ya Umwagiliaji.
_1773804400.jpeg)
Amesema, ili kufanikisha hilo imeanzisha programu ya Mifumo Himilivu ya Chakula inayolenga kuimarisha sekta ya kilimo cha Umwagiliaji, mbegu bora, afya ya udongo pamoja na uhifadhi wa mazao.
Ameongeza kuwa, hatua ya kusainiwa mikataba huo wa usimamizi wa miundombinu katika skimu mbalimbali nchini ni sehemu ya mkakati unaolenga kuhakikisha miradi ya Umwagiliaji inaendeshwa kwa ufanisi na kudumu kwa muda mrefu.
Naye Mwenyekiti wa skimu ya Umwagiliaji ya Ilemba Jimola Nganga, amewataka wakulima kushirikiana na viongozi wa skimu katika kutekeleza mkataba huo ili kuhakikisha mradi unaleta manufaa yaliyokusudiwa kwa wakulima.

Amesema, mkataba huo unalenga kuweka utaratibu wa namna ya kusimamia mradi, kuutunza pamoja na kugawana maji kwa usawa ili kila mkulima aweze kunufaika na uwekezaji huo wa serikali.
Mradi wa Umwagiliaji wa Ilemba unaotekelezwa katika eneo hilo unatarajiwa kunufaisha zaidi ya wakulima 67,0000 kutoka vijiji vya Ilemba A, Ilemba B, Kaswepa na Isanga ambapo tayari zaidi ya hekta mia nane zinaendelea kulimwa kwa kutumia miundombinu ya Umwagiliaji iliyopo.

