Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Tume ya Taifa ya Umwagiliaji

Habari

WAKULIMA WA ITIPINGI WAINGIA MAKUBALIANO NA NIRC YA USIMAMIZI WA SKIMU


 

📍Itipingi, Njombe.

Wakulima wa skimu ya Umwagiliaji ya Twilumba Itipingi wilayani Njombe wamesaini mkataba wa uendeshaji, usimamizi na matunzo ya skimu hiyo kwa kushirikiana na Tume ya Taifa ya Umwagiliaji kupitia Mradi wa Mifumo Himilivu ya Chakula Tanzania (TFRP–P4R).

Mkataba huo unalenga kuimarisha usimamizi wa miundombinu ya umwagiliaji pamoja na kuhakikisha wakulima wanashiriki kikamilifu katika utunzaji na uendeshaji wa skimu ili kuongeza uzalishaji wa mazao.

Akizungumza katika mkutano wa wanachama wa wakulima wa skimu hiyo, Diwani wa Kata ya Igongolo Japheti Myamba amesema wananchi wameupokea mradi huo kwa moyo mmoja na wako tayari kushirikiana na Serikali katika kuutunza.

Amesema, ni muhimu wakulima kuheshimu sheria na taratibu za utunzaji wa vyanzo vya maji ikiwemo kuacha umbali unaotakiwa kisheria na kupanda miti rafiki na maji ili kulinda mazingira ya vyanzo vya maji.

Kwa upande wake Kaimu Mhandisi wa Umwagiliaji mkoa wa Njombe Allen Kimaro amesema Serikali imeanza kuchukua hatua za kuboresha miundombinu ya Umwagiliaji katika skimu hiyo ili kupunguza upotevu wa maji.

Ameeleza kuwa, mfereji wa awali wenye urefu wa mita 1,725 ulioanza kujengwa katika awamu ya kwanza unafanyiwa marekebisho ambapo takribani mita 700 zinafanyiwa ukarabati na baadhi ya sehemu zinajengwa upya kutokana na upokei wa maji.

Kimaro ameongeza kuwa wataalamu pia wamepanga kuweka mifumo ya kuongeza maji katika maeneo ya mwisho ya skimu kupitia visima na vibwawa mtulizo ili kuhakikisha maji yanafika hadi mwisho wa mashamba kama ilivyokusudiwa.

Naye Afisa Kilimo kutoka Tume ya Taifa ya Umwagiliaji Emanuel Lukombeso, amewataka wakulima kuacha kulima karibu na vyanzo vya maji kwa kuwa hali hiyo husababisha mmomonyoko wa udongo na kujaa kwa mchanga kwenye mifumo ya Umwagiliaji.

Amesema, kwa mujibu wa sheria mkulima hapaswi kulima ndani ya mita 60 kutoka kwenye chanzo cha maji pamoja na kuacha umbali wa mita tatu katika mfereji mkuu wa Umwagiliaji ili kulinda miundombinu hiyo.

Akihitimisha mkutano huo, Mwenyekiti wa Chama cha Umwagiliaji skimu ya Twilumba Itipingi, bwana Linus Kisasa, amewashukuru wanachama kwa kupokea maelekezo yaliyotolewa na wataalamu pamoja na kuishukuru Serikali kwa kuwaletea mradi huo.

Amesema utekelezaji wa mradi huo unatarajiwa kuongeza uzalishaji wa mazao na kipato kwa wakulima wa kijiji cha Itipingi na maeneo ya jirani.