Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Tume ya Taifa ya Umwagiliaji

Habari

MATUMIZI BORA YA MAJI YA UMWAGILIAJI YAWEKEWA MKAZO SKIMU YA ITIPINGI



📍Itipingi, Njombe .

Serikali kupitia Tume ya Taifa ya Umwagiliaji imeendelea kuwahimiza wakulima wa skimu ya Umwagiliaji ya Itipingi wilayani Njombe kutumia maji kwa ufanisi pamoja na kushiriki kikamilifu katika usimamizi wa miundombinu ya Umwagiliaji ili kuongeza tija ya uzalishaji wa mazao.

Hatua hiyo inakuja wakati Serikali ikiendelea kuboresha miundombinu ya Umwagiliaji katika skimu hiyo ikiwa ni pamoja na ukarabati wa mifereji pamoja na kuondoa changamoto zilizokuwa zinasababisha upotevu wa maji.

Akizungumza katika mafunzo ya uendeshaji, usimamizi na matunzo ya miundombinu ya Umwagiliaji kwa wakulima wa skimu hiyo, Mhandisi wa Wilaya ya Njombe kutoka Tume ya Taifa ya Umwagiliaji Alfa Jackson, amesema ukarabati wa miundombinu ya Umwagiliaji unaendelea kufanyika ili kuhakikisha maji yaliyopo yanapatikana kwa kutosha kwa wakulima.

Amesema, awali skimu hiyo ilikuwa inamwagilia takribani hekta 60 kwa kutumia mfereji wa mawe wenye urefu wa kilomita 1.725 ambao ulikuwa ukivuja na kusababisha upotevu wa maji.

Ameongeza kuwa, kwa sasa mfereji huo unafanyiwa ukarabati na kujengwa kwa mfumo wa zege pamoja na kusafisha eneo la chanzo cha maji katika mto Fukulu ili kuondoa mchanga na matete yaliyokuwa yakizuia mtiririko wa maji.

Kwa upande wake mkulima wa skimu hiyo Jovita Mkani, amesema changamoto kubwa iliyokuwa inawakabili wakulima katika eneo hilo ni upotevu wa maji kutokana na mifereji iliyokuwa ikivuja jambo lililokuwa linaathiri uzalishaji na kipato cha wakulima.

Amesema, ana matumaini kuwa jitihada zinazofanywa na Serikali katika kuboresha miundombinu ya umwagiliaji zitasaidia kuongeza uzalishaji wa mazao na kuboresha maisha ya wakulima katika eneo hilo.

Naye mkulima na mgawa maji wa skimu ya Itipingi Bonifas Mpinga, amesema licha ya changamoto ndogo za kibinadamu na mabadiliko ya hali ya hewa, wakulima wameendelea kushirikiana na Serikali kuhakikisha mradi huo unaleta manufaa kwa wananchi.

Ameongeza kuwa wakati wa kiangazi mahitaji ya maji huwa makubwa kutokana na kuongezeka kwa idadi ya wakulima wanaohitaji maji ya Umwagiliaji, hali ambayo wakati mwingine husababisha upungufu wa maji katika baadhi ya maeneo ya skimu.

Hata hivyo amesema kazi ya ukarabati wa miundombinu inaendelea kufanyika katika maeneo mbalimbali ya skimu ili kupunguza upotevu wa maji na kuhakikisha maji yanafika mashambani kwa ufanisi zaidi.

Akifafanua kuhusu matumizi bora ya maji, Afisa Maendeleo ya Jamii kutoka Tume ya Taifa ya Umwagiliaji Heaven Jesse amesema mafunzo yanayotolewa kwa wakulima yanawalenga kuwajengea uelewa kuhusu matumizi sahihi ya maji pamoja na umuhimu wa kufuata kalenda ya mazao.

Amesema kupitia mpangilio wa kalenda ya mazao wakulima wataweza kupangilia muda wa kupanda na kuvuna mazao kwa kuzingatia upatikanaji wa maji ili kuhakikisha maji yaliyopo yanatumika kwa ufanisi na kuwafikia wakulima wote.

Aidha amesema Serikali inaendelea kutoa elimu kwa wakulima kuhusu matumizi bora ya rasilimali maji pamoja na usimamizi wa skimu za Umwagiliaji ili kuhakikisha miradi hiyo inakuwa endelevu.

Akihitimisha mafunzo hayo, Mkurugenzi Msaidizi wa Uendeshaji kutoka Tume ya Taifa ya Umwagiliaji Salome Njau, amewataka wakulima kuendelea kushirikiana na Serikali kwa kuchangia ada ya huduma za Umwagiliaji pamoja na kutunza miundombinu ya skimu ili kuhakikisha uwekezaji unaofanywa na Serikali unawanufaisha wakulima kwa muda mrefu.