Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Tume ya Taifa ya Umwagiliaji

Habari

RAIS SAMIA AAGIZA MRADI WA UJENZI WA BWAWA LA UMWAGILIAJI MKOMAZI UKAMILIKE KWA WAKATI


 

NIRC Tanga.

Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, ameeleza kuridhishwa kwake na maendeleo ya mradi wa Umwagiliaji Mkomazi unaotekelezwa na Tume ya Taifa ya Umwagiliaji (NIRC) mkoani Tanga.

Akizungumza wakati wa uwekaji jiwe la msingi la ujenzi wa Bwawa la Umwagiliaji Mkomazi, Dk. Samia amesema kuwa mradi huo uliozungumzwa kwa miaka mingi bila ya kufanyiwa  kazi, lakini sasa serikali imeamua kuujenga na kueleza kuridhishwa na hatua ya ujenzi wa mradi. 

“Ni matarajio yangu kuwa itakapokamilika miradi hiyo kero ya maji itakuwa ni historia huku Lushoto, bwawa hili likikamilika litakuwa na uwezo wa kuingiza maji zaidi ya lita bilioni 70 kwa ajili ya kilimo,”alisema.

Amesema lengo la ujenzi wa bwawa hilo ni kutumika katika shughuli za kilimo na mambo mengine lakini kubwa ni uzalishaji wa mazao ya kilimo.

Rais Samia amesisitiza kuwa Tanzania sasa inajitegemea kwa mazao ya chakula kwa asilimia 128 huku Nchi zinazoizunguka Zikiwa hazijitoshelezi kwa chakula na hivyo kutoa fursa ya Soko la Uhakika kwa Mazao yanayozalishwa nchini.

 “Mabwawa tunayojenga yanakwenda kuongeza eneo la kilimo na kuvuna maradufu ndani ya mwaka mmoja, tunakwenda kufanya Tanzania iwe nchi ya kilimo, Hayati Mwalimu Julius Nyerere alisema kilimo ndio uti wa mgongo tunakwenda kulithibitisha hilo, ombi langu kwenu wananchi ni kushirikiana na wajenzi wa hii miradi,” alisema. 

Kwa Mujibu wa Rais Samia, Mradi wa Ujenzi wa Bwawa la Umwagiliaji Mkomazi utawanufaisha Zaidi ya wananchi elfu 20 kutoka Vijiji 28 vya Kata Saba za Wilaya Korogwe. 

“Nilimpa Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe, sh. bilioni 18.2 kwa ajili ya mradi huu ambao utawezesha kushiriki shughuli za kilimo, wakulima watalima sasa bila kutegemea mvua, ukivuna utasikiliza ushauri wa maofisa kilimo, unaendelea kulima kitu kingine, ili mradi ndani ya mwaka utavuna mara mbili au mara tatu,” alisema.

 Amesisitiza kuwa uwepo wa mradi huo ni ukombozi mkubwa kwa wakulima na amepata faraja, kutokana na kuona waliokuwa hawautaki mradi huo wamekunjua mioyo yao na mradi umeanza kutekelezwa ambapo matumaini yake utamalizika kwa wakati kama ilivyopangwa.

Kwa upande wake Waziri wa Kilimo Husein Bashe, amesema mradi huo unatekelezwa kwa kasi kubwa kama Rais Dkt Samia alivyoagiza na kamwe serikali haitakubali siasa ikatishe utekelezaji wa miradi ya Umwagiliaji.

 

“Tunaishukuru sana Wilaya ya Korogwe na mkoa kwa ujumla,mradi huu ulikuwa na siasa wapo baadhi ya watu walitaka usitekelezwa, tulisimama serikali na kuhakikisha miradi ya maendeleo ambayo ni muhimu kwa jamii inatekelezwa,”alisema.

Waziri Bashe amesema mradi huo ni miongoni mwa miradi 100 ya vipaumbele ya Umwagiliaji ambayo Tume ya Taifa ya Umwagiliaji chini ya Wizara ya Kilimo inaendelea kuikamilisha.

Mradi wa Mkomazi ni wa kihistoria, uliobuniwa zaidi ya miaka 50 iliyopita lakini umekuwa ukisuasua kutekelezwa kwa muda mrefu Kabla Serikali ya Awamu ya sita chini ya uongozi wa Rais Mhe. Dr. Samia Suluhu Hassan kutoa fedha kwa ajili ya kuutekeleza. mradi huo utakaowanufaisha Zaidi ya wananchi elfi 20 kutoka kata saba za Mkomazi, Mkumbara, Mazinde, Mombo, Chekelei, Makuyuni na Magila Gereza.

Mradi huo unagharimu zaidi ya Shilingi Bilioni 18 na unatarajiwa kukamilika ifikapo Agosti 2025. 

Miongoni mwa Kazi zinazotarajiwa kufanyika kwenye Mradi huo ni pamoja na ujenzi wa tuta la udongo la kuzuia maji, ujenzi wa barabara kuelekea eneo la mradi, na ujenzi wa ofisi ya meneja wa mradi.