Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Tume ya Taifa ya Umwagiliaji

Habari

RC MANYARA AZINDUA UCHIMBAJI WA VISIMA VIREFU 40 VYA UMWAGILIAJI


 

NIRC Manyara.

Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Mhe.Queen Sendiga, amezindua uchimbaji wa visima virefu 40 vya Umwagiliaji, katika vijiji 40 vya Wilaya tano za mkoa, kwa lengo la kufikia malengo ya agenda 10/30 na visima hivyo vitaenda kuwanufaisha wananchi zaidi ya 650 kwa awamu ya kwanza na kuongeza usalama wa chakula na kuleta kilimo chenye tija ndani ya mkoa.

Aliyasema hayo wakati akizindua mradi huo wa uchimbaji wa visima virefu 40 vya Umwagiliaji, vya Tume ya Taifa ya Umwagiliaji (NRC), katika kijiji cha Genda kuu wilayani Babati, Oktoba 23, 2025.

Aidha amewataka Wakurugenzi wa Halmashauri na mhandisi wa Tume, Richard Mgaya, wahakikishe kwamba wanasimamia vizuri utekelezaji wa mradi huo, ambao Serikali imeweka fedha nyingi hapo. Na kusema kuwa kama Mkoa katika bajeti ya fedha ya mwaka 2025/26 kuna zaidi ya bilioni 85 ambayo imewekwa kwenye masuala ya Umwagiliaji. Na wakizisimamia vizuri hakika wataiona tija yake.

"Maelekezo yangu, ni ushiriki wa wananchi wenyewe kwenye maeneo yao, pamoja na viongozi wa vijiji ili kuweza kupata tija ya mradi huu. Ni muhimu hawa wataalamu ambao wapo sahizi huku wanaotafuta maeneo kwa ajili ya kuchimba visima, washirikiane na viongozi wa vijiji na wananchi wa kwenye maeneo hayo ili kusikiliza wenyewe wanasemaje kulingana na maeneo yao." Alisema Mhe. Sendiga.

Sambamba na hayo alisema kuwa mitambo mitano ya uchimbaji wa visima, itaanza kufanya kazi katika Mkoa, na mitambo hiyo itafanya kazi kwa siku thelathini (30) zilizopangwa,na kwa awamu ya kwanza itachimba visima 40.

Hata hivyo kwa upande wake Mhandisi Umwagiliaji Mkoa wa Manyara Richard Mgaya amesema mradi unalenga uchimbaji wa visima 40 ambavyo vitamwagilia zaidi ya ekari 1,600 na kunufaisha wakulima zaidi ya 640. Visima hivyo vitachimbwa katika kila wilaya ya mkoa wa Manyara kwa kutumia teknolojia ya kisasa, huku utekelezaji wake ukifanyika kwa ushirikiano kati ya Tume ya Taifa ya Umwagiliaji na Halmashauri husika. Mradi unatarajiwa kukamilika ndani ya kipindi cha mwezi mmoja.

Akifafanua kuhusu utekelezaji, Mhandisi huyo amesema kazi zitakazotekelezwa ni pamoja na utafiti wa kijiolojia ili kuhakikisha upatikanaji wa maji ya kudumu, ambapo kati ya visima 40, tayari visima 32 vimefanyiwa uhakiki wa awali. Kazi nyingine ni uchimbaji wa visima virefu visivyozidi mita 250, uwekaji wa mabomba yenye kipenyo cha inchi 6 hadi 8, usanifu wa mashamba, ufungaji wa pampu, ujenzi wa mnara wa maji pamoja na tanki lenye ujazo wa lita 10,000, na uwekaji wa mabomba ya matoleo ya maji yenye kipenyo cha inchi 3. 

Aidha Mhe. Sendiga amewataka wananchi waongeze ushiriki wao na ushirikiano mkubwa na wataalamu ambao wapo hapa mkoani, lakini pia wailinde miundombinu ya mradi huo na vifaa mbalimbali na kutoa wito wachangamkie fursa ya kilimo lakini pia wakulima wote wajisajili kwenye Tume ya Taifa ya Umwagiliaji ili wafanye shughuli zao kwa kufuata miongozo ya Serikali.