Habari
DKT MASIKA - AWAASA WAKULIMA KUCHUKUA TAHADHARI DHIDI YA ELNINO KWA KUSAFISHA MIUNDOMBINU YA UMWAGILIAJI
📍Skimu ya Mwamkulu, Katavi.
Bodi ya Uongozi ya Tume ya Taifa ya Umwagiliaji (NIRC) imewaasa wananchi na wakulima wa Mkoa wa Katavi kuchukua tahadhari dhidi ya mvua zinazotarajiwa za El-Nino kwa kulinda miundombinu ya Umwagiliaji, huku ikisisitiza wajibu wa kutunza miradi inayogharimu fedha nyingi za Serikali.
Wito huo umetolewa na Mwenyekiti wa Bodi, Mhandisi Dkt. Richard Masika, alipokuwa akizungumza na wananchi wakati wa ziara ya siku Saba ya bodi hiyo lengo ni kukagua maendeleo ya mradi wa skimu ya Umwagiliaji Mwamkulu mkoani Katavi.

Amesema, iwapo mifereji itaachwa bila kusafishwa miongoni mwa athari zinazoweza kutokea ni maji kushindwa kupita kwenye njia yake na kusababisha madhara na uharibifu miundombinu hiyo ya Umwagiliaji ambayo Serikali imetumia fedha nyingi kujenga.
”Viongozi wa maeneo husika na wananchi mshirikiane bega kwa bega na wataalamu wa Tume kujiandaa kikamilifu kudhibiti maji mengi yanayoweza kutokana na mvua za El-Nino ili kuhakikisha miundombinu hiyo haisombwi wala kuharibiwa,”amesema.

Aidha Mhandisi Dkt. Masika amewaasa vijana wazawa waliopata fursa ya kufanya kazi kwenye mradi huo kuhakikisha wanajifunza kikamilifu kutoka kwa wataalamu na mkandarasi, ili waje kutumika kufanya ukarabati na ujenzi wa miradi mingine hapo baadaye bila kutegemea wataalamu kutoka nje.
Vilevile, Dkt. Masika amekemea vikali vitendo vya uharibifu wa miundombinu, ikiwemo kupitisha mifugo na kufungua barabara zisizo rasmi zinazoharibu matuta ya mradi.

Akifafanua ukubwa wa uwekezaji huo, Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Uendelezaji Miundombinu wa NIRC, Mhandisi Leopold Runji, amebainisha kuwa Serikali imetoa zaidi ya Shilingi bilioni 31 kufanikisha ujenzi huo. Ameeleza kuwa kukamilika kwa Skimu ya Mwamkulu kutaongeza ukubwa wa eneo la umwagiliaji kutoka hekta 1,000 zilizokuwepo awali hadi kufikia hekta 3,500, hatua inayokwenda kuleta mapinduzi makubwa ya kilimo na kuongeza tija ya uzalishaji kwa kiasi kikubwa.

Kwa upande wao, baadhi ya wakulima na wakazi wa eneo hilo wameishukuru Serikali kwa uwekezaji huo wa kihistoria unaoenda kubadilisha maisha yao kiuchumi.
Bw. Ezekieli Mathayo Mapolu, mkazi wa Kijiji cha Kabwaga kata ya Mwamkulu, ameeleza kuwa mradi huo unawawezesha kulima kwa uhakika mara mbili kwa mwaka tofauti na zamani walipokuwa wakitegemea mvua pekee, jambo litakaloongeza kipato chao.
Naye Bw. Peter Cosmas Masalu (mkulima), amesisitiza kuwa jukumu lao kuu kama wananchi ni kuutunza na kuulinda mradi huo kwa nguvu zote, akibainisha kuwa ulinzi huo ndiyo njia pekee ya kuishukuru na kuishawishi Serikali kuendelea kufanya uwekezaji zaidi katika eneo lao.

