Habari
MAJI YA UHAKIKA YAFUNGUA UKURASA MPYA WA MAISHA KWA WAKULIMA KILADEDA A
📍Kiladeda A, Meru DC –
Wakulima wa skimu ya Umwagiliaji Kiladeda A wameanza kuona mwelekeo mpya wa maisha kufuatia kuingia makubaliano ya usimamizi, uendeshaji na matunzo ya miundombinu ya Umwagiliaji kati yao na Tume ya Taifa ya Umwagiliaji.
Hatua hiyo inalenga kuimarisha upatikanaji wa maji, kuongeza uzalishaji na kuinua kipato cha wakulima.
Akizungumza mkulima wa skimu hiyo, Vincent Mushi, amesema ujio wa maji ya uhakika utaongeza uzalishaji kutoka kiwango cha chini hadi mavuno yenye tija zaidi, huku akibainisha kuwa mafanikio hayo yatawezesha familia kumudu gharama za maisha ikiwemo elimu ya watoto na kuboresha makazi. Aidha, ameahidi kuwa wakulima wako tayari kuchangia ada ya huduma ya Umwagiliaji ili kuhakikisha uendelevu wa skimu.
_1792576211.jpeg)
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa skimu hiyo, Cornel Mushi, amesema makubaliano hayo ni matokeo ya jitihada za muda mrefu za wakulima waliotafuta suluhisho la changamoto zao, akisisitiza kuwa sasa ni wajibu wa wanachama kubadilisha mtazamo na kufuata taratibu za kitaalamu ili kufikia malengo ya uzalishaji wa kisasa na wenye tija.
Akieleza upande wa kitaalam, Afisa Kilimo kutoka Tume ya Taifa ya Umwagiliaji, Emmanuel Lukombeso, amesema maboresho yatakayofanyika kwenye miundombinu mikubwa kama banio na mfereji mkuu yatahakikisha maji yanawafikia wakulima wote kwa usawa, jambo litakalowezesha kila mkulima kunufaika na kuongeza uzalishaji.
_1792576287.jpeg)
Akihitimisha, Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Uendeshaji kutoka Tume ya Taifa ya Umwagiliaji, Salome Njau, amesisitiza umuhimu wa wakulima kusajiliwa rasmi kwenye mfumo wa usimamizi wa umwagiliaji pamoja na kuendelea kuchangia ada ya huduma ili kuwezesha uendeshaji na matengenezo ya miundombinu, akibainisha kuwa ushirikiano huo ndio utakaohakikisha miradi inakuwa endelevu na kunufaisha wengi zaidi.
Mradi huo unatekelezwa kupitia Programu ya Mifumo Himilivu ya Chakula Nchini (TFSRP), inayofadhiliwa na Benki ya Dunia kwa kushirikiana na IFAD, ukiwa na lengo la kuimarisha kilimo cha Umwagiliaji na kukabiliana na changamoto za mabadiliko ya tabia ya nchi.


