Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Tume ya Taifa ya Umwagiliaji

Habari

WAKULIMA WAASWA KULINDA MIUNDOMBINU YA UMWAGILIAJI


📍NIRC Singida.

Bodi ya Uongozi Tume ya Taifa ya Umwagiliaji imetoa wito kwa wakulima nchini kulinda miundombinu na kuchangia ada za huduma za Umwagiliaji kwa ajili ya ukarabati na uendelezaji miundombinu hiyo, huku ikitoa ushauri kwa wataalamu wa Tume kuweka mipaka ya hifadhi (Buffer Zones) katika mabwawa yote ili kuzuia shughuli za kibinadamu zinazochangia kupungua kwa kina cha bwawa.

Wito huo umetolewa na Mwenyekiti wa Bodi hiyo, Mhandisi. Dkt. Richard Masika, wakati wa ziara ya kukagua miradi ya Umwagiliaji ikiwemo skimu ya Umwagiliaji Masimba na skimu ya Msingi zilizopo wilaya ya Iramba na Mkalama mkoani Singida.

Akitolea ufafanuzi suala la mipaka, Dkt. Masika ameeleza kuwa kumekuwa na dhana miongoni mwa wananchi wanaodhani kuwa mradi unaishia kwenye kingo za maji, ili kuondoa changamoto hiyo, amewaagiza wataalamu kuweka alama za wazi zinazoonyesha ukomo wa bwawa ambao hauruhusiwi kufanyiwa shughuli zozote za kibinadamu bila idhini.

Akigusia umuhimu wa utunzaji wa miundombinu, Dkt. Masika amesisitiza kuwa mradi wa Umwagiliaji ni sawa na mtoto anayehitaji kulelewa, hivyo amewasihi wakulima kutimiza wajibu wao wa kuchangia ada za huduma za Umwagiliaji, kwani fedha hizo ndizo zitatumika kugharamia matengenezo na ukarabati wa miundombinu hiyo pindi inapopata hitilafu.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Taifa ya Umwagiliaji, Bw. Raymond Mndolwa, amesema Tume itashirikiana na viongozi wa ngazi za chini wakiwemo viongozi wa skimu, madiwani kufanya uhamasishaji na kutoa elimu kwa wananchi ili waache kufanya shughuli za kibinadamu zinazosababisha kujaa kwa matope kwenye mabwawa.

Bw. Mndolwa amefafanua kuwa tatizo kuu linalobaki na kuathiri mabwawa ni matope ambayo yanatengenezwa moja kwa moja na shughuli za binadamu. "Elimu  hii ni muhimu sana kwa jamii ili waweze kuelewa namna shughuli za kibadamu kando ya bwawa zinavyochangia kuharibu miundombinu, hivyo wachukue hatua za makusudi kulinda mabwawa hayo yasijae matope,"amesema.

Baadhi ya wakulima wa skimu ya Umwagiliaji ya Masimba akiwemo Chosela Mkumbo na Erekto Shinyara, wameishukuru Serikali kwa kufufua mradi huo wa kihistoria ambao uliasisiwa tangu enzi za ukoloni. Wakulima hao wameeleza kuwa, kwa muda mrefu walihangaika sana kutokana na uhaba wa maji na kuambulia mavuno kidogo, lakini ujenzi wa sasa unaofanywa utawawezesha kupata mavuno ya kutosha na kunufaisha zaidi ya wananchi 24,000 pamoja na vizazi vyao.

Aidha, wakulima hao wameunga mkono maagizo ya viongozi kwa kuahidi kuendelea kuhamasishana wenyewe kwa wenyewe kuchangia ada ya huduma za Umwagiliaji, ili kusaidia utunzaji wa miundombinu hiyo na kuiwezesha Serikali kupata fedha za kupeleka miradi kama hiyo katika maeneo mengine nchini.

Kukamilika kwa miradi hii kutaleta mapinduzi ya kiuchumi mkoani Singida ambapo skimu ya Msingi itatoa hekta 800 zitamwagiliwa, kuwezesha kilimo cha misimu yote na kunufaisha wananchi zaidi ya 12,000, huku skimu ya Masimba itamwagilia hekta 750 za mpunga, mahindi na mbogamboga, ikinufaisha wananchi zaidi ya 24,000. Kupitia utekelezaji huu, Tume inatimiza kwa vitendo azma ya Serikali ya kuimarisha usalama wa chakula na kuinua vipato kupitia kilimo cha uhakika.

slot gacor