Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Tume ya Taifa ya Umwagiliaji

Habari

UJENZI SKIMU YA LUICHE: WANANCHI WATAKIWA KUPEWA KIPAUMBELE


<Mwenyekiti wa bodi NIRC, asisitiza wajibu wa ulinzi wa mradi upo kwao, Mkandarasi aagizwa kuzingatia Ubora

 

📍Skimu Luiche, Kigoma.

 

Wananchi wa Mkoa wa Kigoma wameaswa kupokea, kutunza na kuulinda mradi wa skimu ya Umwagiliaji ya Luiche kwa kuwa ni mali yao iliyojengwa kwa fedha za Serikali.

Sambamba na hilo, wasimamizi na wakandarasi wa mradi huo wameaswa kuhakikisha wanazingatia ubora wa kiwango cha juu ili uwekezaji huo uendane na thamani ya fedha zinazotumika.

Wito huo umetolewa na Mwenyekiti wa Bodi ya Uongozi ya Tume ya Taifa ya Umwagiliaji (NIRC), Mhandisi . Dkt. Richard Masika, wakati wa ziara ya kukagua maendeleo ya mradi huo uliopo katika Wilaya ya Kigoma Ujiji, ambapo amesisitiza umuhimu wa ushirikishwaji wa Jamii katika ujenzi huo na kuwapo kwa mahusiano mema kati ya viongozi, wataalamu wa mradi na jamii inayowazunguka.

Dkt. Masika ameitaka timu ya usimamizi ikiongozwa na Mhandisi wa Mkoa na wataalamu wa ushauri kufanya kazi kwa ukaribu na wananchi ambao ndio wanufaika wa mradi huo.

“Wamilikisheni wananchi mradi huu, huu ni mradi wao unaojengwa kwa fedha nyingi za umma ambazo ni kodi zao, lazima wahakikishe wanautunza na kuulinda na kuusimamia ipasavyo sisi tupo hapa kwa niaba ya Serikali tutamaliza tutaondoka wao ndio wanufaika,”amesema

Pia, ametoa agizo kwa mkandarasi kuhakikisha kuna uwepo wa maabara ya kupima vifaa vya ujenzi katika kambi yake, pamoja na kupima na kuthibitisha ubora wa vifaa vyote vinavyotumika kwenye eneo la ujenzi kila wakati ili kukidhi viwango vinavyotakiwa.

Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Uendelezaji Miundombinu wa NIRC, Mhandisi. Leopold Runji, amesema mradi wa skimu ya Luiche unatekelezwa kwa sehemu mbili ambazo ni ujenzi wa bwawa na ujenzi wa miundombinu ya mifereji.

Amesema kazi zinaendelea vizuri huku ujenzi wa mfereji mkuu wenye urefu wa zaidi ya kilomita tano umeshaanza na maandalizi ya kambi ya mkandarasi yamekamilika kwa kiwango kinachotakiwa.

Kwa upande wake, Mhandisi wa Umwagiliaji Mkoa wa Kigoma,. Mustang Katuta, amebainisha kuwa mradi huo unakwenda kubadilisha sura ya kilimo mkoani humo,

 “Bwawa litakuwa na ujazo wa mita za ujazo 710,000 ambapo mradi una uwezo wa kumwagilia hekta 3,000 huku zaidi ya wakulima 9,500 wanatarajiwa kunufaika moja kwa moja,”amesem. Pia aliongeza kuwa uzalishaji wa mazao ya chakula, ikiwemo mpunga na zao la kimkakati la Chikichi, utaongezeka kwa kiasi kikubwa ndani ya mkoa huo.

Baadhi ya wakulima wa eneo hilo akiwemo Bi. Amissa Ndarugiliye na Bi. Halima Maulidi Salama wamemshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwaletea kilimo bora kinachotatua changamoto za muda mrefu na kukiri kuwa kukamilika kwa mradi huo ni ufunguo utakaowawezesha kuongeza mavuno na kukuza biashara ya kilimo.

slot gacor